Wezesha

kama una maoni au habari tafadhali tutumie kwa kupitia email yetu.shanellally@gmail.com

Afya

UMRI WA KUZAA
Tamaa ya kutaka kufanikiwa maishani imeenea duniani kote. Hali imebadilika sana, jinsia ya kike inataka kujitosheleza kwa kila kitu. Lakini mabadiliko ya kibaiolojia yanabaki vile vile mfano kuzeeka nk.
Mafanikio wanayowaza wengi ni utajiri wa pesa na elimu kubwa. Hii imesababisha wanawake wengi kusoma sana na kufanya kazi kupita kiasi, hata kupuuzia suala la kuzaa mapema.

Wengi wanashtuka ikiwa umri wao ni zaidi ya miaka 30, ndio wanakuwa na tamaa ya kuzaa. Kuchelewa kwao kuzaa kunaweza kuwa kwa taabu ama kuzaa watoto wenye matatizo mengi ya kiafya.
Kwa miaka mingi, wataalamu wengi wa afya ya uzazi bado wanaamini miaka 20-35 ndio umri sahihi kushika mimba na kuzaa.
Pia, wengi wakifikiri matatizo mengi ya uzazi huongezeka baada ya miaka 35 na huwa zaidi baada ya miaka 40.
Kwa wenzi wawili wanaoishi pamoja, kuchelewa kuzaa huathiri pia wenza wa kiume, ambapo mbegu za uzazi za mwanaume hudhorota kila mwaka upitao na watoto wamaotokana na wanaume wazee huwa na hatari zaidi ya kupata matatizo ya akili na matatizo ya chembe za urithi.
KUBALEHE
Kubalehe ni hatua muhimu sana lupotia ili kuweza kuzaa. Wastani wa kubalehe na kuvunja ungo kwa wasichana ni miaka 9-12 kwa sasa, ingawa miaka ya zamani ilikuwa kuanzia miaka 12-14.
Baada ya kubalehe binti anakuwa na uwezo wa kushika mimba, japokuwa uwezekano huongezeka zaidi kati ya miaka 20-30, baada ya hapa uwezekano huanza kupungua.
Kulingana na The American College of Obstricians & Gynecologists uwezo wa wanawake kuzaa hupungua katika umri wa miaka 32 na hupungua kwa kasi zaidi katika umri wa miaka 37.
Uwezo wa wanawake kuzaa hupungua vile umri unaongezeka kwa kuwa wanawake wanapobalehe wanakuwa na idadi kamili ya mayai katika ovari zao. Namba hii hupungua vile mwanamke anavyozeeka. Pia mayai hayazalishwi kiurahisi kwa wanawake wenye umri mkubwa ukilinganisha na mabinti wadogo.
Kulingana na National Institute for Health & Clinical Excellence (NICE) ya Umoja wa madola (UK), kwa wanawake wenye miaka 35, ni wanawake 94 kati ya 100 wanaweza kupata ujauzito wakifanya ngono kwa ukawaida ndani ya miaka 38, ni wanawake 77 kati ya 100 wanaweza kushika ujauzito.
Magonjwa ya njia za uzazi kama Endometriosis na Uterine fibroids yanawatokea zaidi wanawake wenye umri mkubwa ambayo husababisha mwanamke kutoshika mimba.
Wanawake wenye umri zaidi ya miaka 35 wanaoamua kushika ujauzito wanakabili hatari ya kupanda kwa shinikizo la damu. Kupanda kwa shinikizo la damu wakati wa ujauzito huathiri kondo la nyuma (Placenta) ambalo hutoa lishe kwa kijusi (kitoto kilicho tumboni) hali ambayo huathiri moja kwa moja ukuaji wake.
Pia, hatari ya kupata kisukari kwa wanawake wanaoshika ujauzito wakiwa na miaka 35 na zaidi, huongezeka sana. Kisukari kipindi cha ujauzito huongeza hatari ya kutoka mimba (Miscarriage), kuzaa mtoto mwenye kasoro au kuzaa mtoto mkubwa kupita kiasi.
TAFITI YA HIVI KARIBUNI
Jambo la kushtusha, ni matokeo ya utafiti uliofanyika Sweden, watafiti wanadai hatari ya matatizo ya uzazi huanza mapema tu pale mwanamke anapofikisha miaka 30.
Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la magonjwa ya uzazi (Journal of Obstetrics & Gynacology) uliofanywa na watafiti kutoka Taasisi ya Karolinska ya nchini Sweden umegundua katika nchi tajiri duniani wanawake huzaa wakiwa na umri mkubwa kitu kinachopelekea kuongezeka kwa hatari ya kuzaa watoto njiti (Preterm birth), ukuaji hafifu wa vichanga na kuzaa watoto wafu (Stillbirth).
Ili kubainisha hatari kati ya makundi tofauti ya umri ya wanawake wanaozaa kwa mara ya kwanza, watafiti walitumia takwimu za vizazi toka hospitali za Sweden na Norway, zilizokusanya taarifa za karibu wanawake milioni moja, kati ya mwaka 1990 na 2010.
Hatari ya kuzaa watoto njiti (Premature birth) na kuzaa watoto wafu huongezeka kuanzia miaka ya 30 ingawa toka zamani, miaka 35 ndio ilitambulika kuwa mwanzo wa hatari kwa wanawake kupata watoto, lakini utafiti huu mpya unataja mwanzo tu wa miaka 30 hatari ya kupata matatizo katika uzazi huanza.
Kwa kulinganisha kati ya kundi la umri wa miaka 25-29 na 30-34, wanawake wa miaka 30-34 wenye mimba za kwanza walikuwa na hatari ya kuzaa watoto njiti kwenye wiki 22-31 za ujauzito au kuzaa watoto wafu.
Kikosi cha watafiti kiligundua pia sababu zingine zinazoweza kuleta matatizo ya uzazi mfano wa sababu hizo ni kama kuvuta sigara au kuwa mnene kuliko kawaida.
Ulla Waldenstrom, profesa wa kitengo cha afya ya wanawake na watoto katika taasisi ya Karolinska alisema : 'Tumeshangazwa na kuongezeka kwa hatari za uzazi katika umri mdogo sana.'
Prof. Waldenstrom aliendelea ; 'Wanawake wanaweza ona hatari ni ndogo ila kwa jamii kiujumla kuna idadi kubwa ya matatizo yasiyo ya lazima kwao wanawake wanaozaa baada tu ya miaka 30. Hivyo nashauri wanawake na wanaume wapewe taarifa mashuleni juu ya umuhimu wa umri katika uzazi.'
Alipoombwa ushauri kwa wanawake wenye umri zaidi ya miaka 30 wanaotaraji kuzaa, Prof. Waldenstrom alisema ; 'Ushauri bora ni kuepuka uvutaji wa tumbaku/sigara na kuepuka unene, kama inawezekana.''
KIPINDI CHA KUKOMA HEDHI (MENOPAUSE)
Wataalamu wa afya wanasema kwamba mwanamke amekoma hedhi anapokosa kupata hedhi kwa miezi 12 mfululizo. Ni wanawake wachache hukoma kupata hedhi ghafula, yaani, wanakosa hedhi mwezi mmoja unakuwa mwisho wa kuipata.
Wanawake wengi huanza kipindi hiki wakiwa na umri wa miaka 40 na kitu, lakini kwa wengine huanza wakiwa wamechelewa wakiwa na miaka 60 na kitu.
Kutokana na mabadiliko ya kiwango cha homoni kinachotokezwa, huenda mwanamke akakosa kupata hedhi pindi kwa pindi, akapata hedhi wakati ambao hakutarajia au akavuja damu nyingi isivyo kawaida wakati wa hedhi. Pia huenda mwanamke akashuka moyo, hisia zake zikabadilikabadilika na hilo linaweza kumfanya alielie bila sababu, na pia asiwe makini sana na asahau mambo.
Kipindi cha kukoma hedhi huwa tofauti kwa kila mwanamke. Dalili zinaweza kuonekana kipindi hicho ni pamoja na joto la ghafula mwilini, ambalo huenda likafuatiwa na kuhisi baridi. Dalili hizo zinaweza kumfanya mtu akose usingizi na kuishiwa na nguvu.
Baadhi ya wanawake hupatwa na joto la ghafla mwilini kwa mwaka mmoja au miaka miwili wakati wa kipindi hicho cha kukoma hedhi.
Wengine hupatwa na hali hiyo kwa miaka mingi na wachache sana husema kwamba wao hupatwa na joto la ghafula mara kwa mara maisha yao yote.
Ni busara mtu afanyiwe uchunguzi wa kiafya kabla ya kuamua kwamba joto la ghafula linasababishwa na kukoma kwa hedhi. Kwa kuwa kuna matatizo mengine ya kiafya yanaweza kuleta joto la ghafula mfano ugonjwa wa dudumio, malaria, homa ya matumbo n.k
JINSI YA KUISHI VIZURI KIPINDI HICHO
Mabadiliko ya mtindo wa maisha yanaweza kupunguza baadhi ya matatizo hayo mfano kuacha kuvuta sigara, kupunguza au hata kuacha kunywa vileo, vinywaji vyenye kafeini na vyakula vyenye sukari au vikolezo ambavyo vinaweza kusababisha joto la ghafula mwilini.
Kufanya mazoezi husaidia sana kupunguza matatizo yanayohusianishwa na kukoma kwa hedhi. Kwa mfano, mazoezi yanaweza kupunguza kukosa usongizi na kusaidia kuboresha hali ya kihisia na pia huimarisha mifipa na afya ya mtu kwa ujumla.
Ili kumsaidia mwanamke kukabiliana vizuri na kipindi hicho cha kukoma kwa hedhi, huenda madaktari wakampa homoni, vitamini na madini, na dawa za kutibu kushuka moyo.
Pia ni jambo la busara kuwaambia uwapendao hali unayokabili ili wakuonyeshe upendo na wakupe msaada unaouhitaji wakati wa hali yako.
Kipindi hicho kinapokwisha, wanawake ambao hutunza afya yao, wanapata tena nguvu na kuendelea kufurahia maisha.

UGONJWA WA KIFUA KIKUU NA DALILI ZA KIFUA KIKUU

Kifua kikuu ni ugongwa unaosababishwa na vimelea vidogo vidogo aina ya bakteria viitwavyo Microbacteria tuberculosis. Ugonjwa wa kifua kikuu unaenezwa kwa njia ya hewa kutoka katika mtu ambaye anaugua na hajaanza matibabu, mtu huyu akipiga chafya, kukohoa au kutema makohozi ovyo anaweza kuambukiza watu wengine.
Kifua kikuu kwa kawaida kinaathiri mapafu, pia kinaweza kuathiri sehemu yeyote ile nyingine ya mwili ikiwemo mifupa, tumbo na mgongo.
Dalili za kifua kikuu ni pamoja na kukohoa kwa wiki mbili au zaidi mfululizo, homa za mara kwa mara kwa wiki mbili au zaidi, kutokwa na jasho jingi hasa nyakati za usiku, kukohoa makohozi yenye damu, kupungua uzito zaidi ya kilo 3 ndani ya wiki 4 au kukonda pamoja na kukosa hamu ya kula.
Kifua kikuu hugundulika kwa kupima makohozi na ikibidi x-ray na matibabu yake ni bure katika hospitali zote za serikali na binafsi. Unapoona mtu ana dalili mojawapo kati ya hizi au wewe mwenyewe mshauri awahi kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na tiba au awasiliane na mratibu wa kifua kikuu na ukoma aliye karibu nae kwani mtu mmoja huweza kuwaambukiza watu kati ya 10 hadi 15 kwa mwaka kama hajapata matibabu. Wastani wa watu 176 huugua kifua kikuu kila siku nchini Tanzania na wastani wa watu 12 hufariki dunia kila siku .
Ikitokea umegundulika kuwa una kifua kikuu usihofu kwani kinatibika na mamilioni ya watu duniani kote wameugua na kupona. Unachotakiwa kufanya ni kufatisha masharti utakayopewa na daktari kama; kunywa dawa kila siku kwa muda uliopangiwa ili kupona kabisa. Matibabu yake huchukua kati ya miezi sita hadi minane.
Endapo umegundulika kuwa na kifua kikuu kumbuka kufunika mdomo na pua unapo kohoa au kupiga chafya, ili usiambukize watu wengine na pia usiteme mate ovyo.
Pumzika kiasi cha kutosha, kula chakula bora na uwafahamishe ndugu na marafiki kwamba unaugua kifua kikuu na uko kwenye matibabu, na ukisha kamilisha matibabu nenda kwa mhudumu wa afya kwa uchunguzi ili kuthibitisha kama umepona.
Kumbuka ni muhimu kuendelea kutumia dawa mpaka mwisho hata kama unajisikia vizuri ili usipate kifua kikuu sugu ambacho matibabu yake ni magumu. Mara wa mara kifua kikuu kimekuwa kikihusishwa na ugonjwa wa ukimwi kwani asilimia 50 ya watu wenye kifua kikuu wana VVU. Kama umethibitika una kifua kikuu ni muhimu kupata ushauri nasaha na kupima virusi vya UKIMWI, kwani asilimia 10-15 ya watu wanaoishi na VVU wanaugua kifua kikuu, hivyo ni muhimu kuchunguzwa kama una kifua kikuu ili kuboresha na kuokoa maisha yako kwani kifua kikuu kinatibika kabisa hata kama una maambukizi ya VVU.


 IJUE KASWENDE (Syphilis)
Ugonjwa wa kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum. Ugonjwa huu ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayoongoza kwa kusababisha madhara mengi. Maambukizi ya kaswende wakati wa ujauzito huleta madhara mengi sana kama vile kujifungua kiumbe ambacho kimeshakufa, mtoto kuathirika na ugonjwa huu wakati wa kuzaliwa, mtoto kupata matatizo wakati wa ukuaji wake, degedege na kuongezeka kwa vifo vya watoto wachanga. Ugonjwa wa kaswende huathiri zaidi ya mimba milioni moja duniani kote kila mwaka na kuchangia theluthi mbili ya vifo vya watoto wanaozaliwa wakiwa tayari wameshakufa katika nchi za maeneo ya chini ya Jangwa la Sahara. Asilimia 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende huishia watoto kufariki wakati wa kuzaliwa. Pia asilimia nyingine 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende husababisha watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu kupata matatizo ya ukuaji, degedege na kuongezeka vifo vya watoto kwa asilimia 50. Kwa mfano Taasisi ya kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania (Tanzania National AIDS Control Programme) au NACP katika ripoti yake ya utafiti uliofanywa chini ya Wizara ya afya na ustawi wa jamii nchini humo ilitangaza kuwa, maambukizi yote ya kaswende wakati wa ujauzito Tanzania bara kati ya mwaka 2003 hadi 2004 yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.7 kwa ujumla, kuanzia mkoani Kilimanjaro ambako maambukizi yalikuwa ya asilimia 0.4 hadi mkoani Tabora ambako yalikuwa ya asilimia 32. Magonjwa ya Ukimwi na kaswende mara nyingi huambatana pamoja ambapo pia ugonjwa wa zinaa wa kaswende huongeza uwezekano wa mtu kupata Ukimwi. Je, ugonjwa wa kaswende huambukizwa kwa njia gani? Kama tulivyosema awali, kaswende husababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum. Njia za maambukizi za ugonjwa huu ni kama zifuatavyo: 1) Kupitia kujamiana bila kutumia kinga au ngono zembe na mtu aliyeambukizwa kaswende. 2) Mama aliyepata ugonjwa wa kaswende wakati wa ujauzito anaweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito. 3) Kuambukizwa kupitia michibuko au mipasuko kwenye ngozi wakati wa kujamiana au wakati mwingine pale mtu anapogusana na mtu mwenye kaswende ikiwa wote wawili wana mipasuko kwenye sehemu mbalimbali za ngozi zao. Sio rahisi mtu kutambua kama ana michibuko au la kwenye ngozi kwani mingine huwa midogo sana isipokuwa ile inayoweza kuonekana kwa macho, lakini huweza kuwa njia ya maambukizo. Baada ya kujua visababishi vya ugonjwa huo sasa tuzibainishe pia dalili zake. Dalili na viashiria vya ugonjwa wa kaswende hutegemea aina ya ugonjwa wa kaswende wenyewe. Kuna aina tano za ugonjwa wa kaswende ambazo ni; Ugonjwa wa kaswende wa awali (Primary syphilis)Ugonjwa wa kaswende wa pili (Secondary syphillis)Kaswende iliyojificha (Latent syphilis)Kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis)Kaswende ya kurithi (Congenital syphilis) Kaswende ya awali (primary syphilis):Dalili ya kwanza ya aina hii ya kaswende ni kutokea kwa kidonda kidogo cha mviringo (chancre kama kinavyojulikana kitaalamu) katika sehemu ambayo bakteria wameingilia na hutokea kati ya siku 10 hadi miezi mitatu (kwa kawaida kuanzia wiki 2 hadi 6) baada ya mtu kupata maambukizi. Kidonda hiki kinaweza kutokea kwenye sehemu ya haja kubwa, shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mdomoni, katika uume, ulimi, vulva, tupu ya mwanamke na sehemu nyinginezo mwilini. Tezi (lymph nodes) ambazo zipo karibu na sehemu iliyotokea kidonda hiki kawaida huwa zinavimba baada ya siku 7 hadi 10. Kidonda hiki hakiambatani na maumivu na kwa kuwa kinaweza kutokea katika sehemu zilizojificha kama kwenye shingo ya kizazi, sio rahisi mtu kutambua kama ana aina hii ya kaswende. Kidonda hiki kinaweza kuwepo kwa muda wa wiki 3 hadi 6 kama mtu hatapata matibabu na hutoweka chenyewe bila tiba au baada ya kupata tiba. Robo tatu ya wale ambao hawapati tiba huishia kuingia kwenye kundi la kaswende ya aina ya pili yaani Secondary syphilis. Aina hii hutokea wiki 4 hadi 10 baada ya mtu kupata kaswende ya awali. Dalili za aina hii ya kaswende ni: vipele ambavyo haviwashi katika viganja vya mikono au nyayo za miguu. Vipele hivi pia vinaweza kutokea mwili mzima au sehemu mbalimbali za mwili. Pia muathirika huhisi uchovu, kuumwa kichwa, homa, kunyofoka nywele, vidonda vya koo, kuvimba kwa matezi mwili mzima, maumivu ya mifupa na kupungua uzito. Kaswende ya aina hii hujitokeza kwa wiki kadhaa na hutoweka hata bila kupata tiba kwa mtu aliyeathirika. Pia inaweza kujirudia rudia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili na mtu huingia kwenye kundi la aina ya tatu ya ugonjwa wa kaswende yaani (latent syphilis) baada ya miaka miwili. Wapenzi wasikilizaji baada ya kuijua kaswende ya aina ya awali na ya pili, tunasonga mbele na kipindi chetu kwa kuelezea kaswende iliyojificha (Latent syphilis). Aina hii inajulikana kama kaswende ambayo inaweza kuthibitika tu kwa kutumia vipimo vya maabara (serological test) na imegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni kaswende iliyojificha ya awali au (Early latent syphilis) kwa kimombo. Hii ni kaswende ambayo hutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya muathirika kuugua kaswende aina ya pili .Aina hii huwa na dalili zinazojirudia kama za kaswende ya pili. Kundi la pili ni kaswende iliyojificha ya kuchelewa au Late latent syphilis. Hii hutokea baada ya mwaka mmoja wa kuugua kaswende ya aina ya pili (secondary syphilis). Wakati wa kuugua aina hii ya kaswende, muathirika huwa hana dalili wala viashiria vyovyote vile na uwezo wake wa kuambukiza mtu mwingine huwa chini au hawezi kabisa kumuambukiza ugonjwa huu mtu mwingine. Kaswende ya aina ya nne kama tulivyosema inaitwakaswende ya baadaye (Tertiary syphilis). Asilimia 30 ya wagonjwa wa kaswende ambao hawakupata tiba hapo awali huingia kwenye kundi hili na hutokea miaka 15 hadi 30 baada ya maambukizi ya kaswende. Aina hii inaweza kuathiri viungo kama macho, ubongo, mishipa ya fahamu, viunganishi vya mifupa au joints, uti wa mgongo, moyo na mishipa ya damu. Kwa ajili hiyo aina hii ya kaswende ni yenye madhara makubwa kwani huweza kusababisha upofu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya akili na magonjwa ya mishipa ya fahamu. Huweza kumfanya mtu kuwa kiziwi na kupungukiwa na kumbukumbu na hata kumsababishia kifo. Pia aina hii ya kaswende inaweza kuathiri mfumo wa chakula, mfumo wa kupumua na mfumo wa uzazi. Wapenzi wasikilizaji kaswende ya aina ya mwisho ni ya kurithi (Congenital syphilis). Aina hii ya kaswende hutokea wakati wa ujauzito au baada ya mtoto kuzaliwa. Nusu ya wototo wanaozaliwa huwa hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huu. Nusu ya watoto wenye maambukizi ya kaswende hufariki dunia muda mfupi kabla ya kuzaliwa au baada ya kuzaliwa. Dalili za aina hii ya kaswende kwa mtoto mchanga zinaweza kutokea baada ya kuzaliwa au wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa. Dalili hizo ni, kutoongezeka uzito au kushindwa kukua, homa, kukasirika haraka, kutochongoka kwa pua yaani pua linakuwa bapa, vipele kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo ambavyo huwa ni vipele vya rangi ya madini ya shaba kwenye uso, viganja vya mikono na nyayo na vipele kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu ya haja kubwa. Dalili nyingine ni kutokwa na majimaji puani, kuongezeka ukubwa wa ini na bandama, ngozi kuwa ya njano, na upungufu wa damu mwilini (anemia). dalili za ugonjwa wa kaswende kwa mtoto mkubwa ambazo ni,kuathirika meno (Hutchinson teeth), maumivu ya mifupa, kupata upofu, kupungua uwezo wa kusikia au mtoto kuwa kiziwi na kuwa na ukungu kwenye mboni za macho (Clouding of cornea). Dalili nyingine ni kutokwa vidonda vya rangi ya kijivu kwenye sehemu ya haja kubwa na kwenye tupu ya mwanamke, ngozi kuwa na mabaka meusi kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu za haja kubwa, maumivu kwenye mikono na miguu na pia kuvimba jointi za mifupa.

1 comment:

  1. Sikuamini kuwa ningeweza kuungana tena na mpenzi wangu wa zamani, nilipatwa na kiwewe cha kusimama peke yangu bila mwili wa kusimama na kuwa nami, lakini nilipata bahati sana siku moja nilikutana na Dk DAWN, baada ya kumwambia. kuhusu hali yangu alifanya kila liwezekanalo kumuona mpenzi wangu anarudi kwangu, kiukweli baada ya kunifanyia uchawi mpenzi wangu wa zamani alirudi kwangu chini ya masaa 48, mpenzi wangu wa zamani alirudi huku akiniomba kuwa hatoniacha kamwe. tena. Miezi 3 baadaye tulioana na kuoana, ikiwa una hali sawa. Ana nguvu nyingi katika mambo yake;
    * upendo
    inaelezea * inaelezea kivutio
    * kama unataka ex wako nyuma
    *acha talaka
    * kuvunja obsessions
    * huponya viharusi na magonjwa yote
    * uchawi wa kinga
    *Ugumba na matatizo ya ujauzito
    * bahati nasibu
    * uchawi wa bahati
    Wasiliana na Dk Ediomo kwenye barua pepe yake: dawnacuna314@gmail.com
    Whatsapp:+2349046229159

    ReplyDelete