UKAWA WAPINGA MAONI YA KATIBA

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
vimetangaza rasmi kutoshiriki katika mchakato wa kura ya maoni ya katiba
na kwamba kuanzia sasa vitahamasisha wananchi kuunga mkono.Uamuzi huo umetolewa leo na wenyeviti wa vyama
wanaounda umoja huo wa ukawa ambao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Makaidi.Akizungumza wakati wa kutoa msimamo huo Profesa
Lipumba amesema wamefikia uamuzi wa kutoshiriki katika zoezi hilo kwa
sababu mchakato mzima haukuwa na maridhiano ya kitaifa.“Vyama vya siasa ikiwemo CCM vilikubaliana mwaka
jana kwamba zoezi la kura za maoni lifanyike mwaka 2016 baada ya
uchaguzi mkuu, tulisaini wote na Rais Jakaya Kikwete alikubali, kwa nini
mabadiliko yafanyike ghafla” amehoji Profesa Lipumba.Amesema jambo la kushangaza, Rais Kikwete aligeuka
na kutangaza kwamba Aprili 30, mwaka huu kuwa siku ya kupiga kura ya
maoni kuhusu Katiba Mpya.Amesema pamoja na kutangaza siku ya kupiga kura,
bado uandikishaji katika daftari la wapiga kura haujaanza kwa sababu
wanasubiri vifaa.“Hadi sasa vifaa vya Biometric Voter Registration
(BVR) vilivyopo ni seti 250 wakati vinavyohitajika ni seti 7500, tume
inasubiri hadi sasa, zoezi hili litafanyika kweli?,” alihoji Lipumba.“Mbinu hiyo inafanywa na Serikali kwa sababu Wazanzibari ndiyo wanaona kikwazo kwao,” alisema Makaidi.Aprili 16 mwaka jana, Wabunge wa Bunge Maalum la
Katiba kutoka vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD walitoka nje
wakidai bunge hilo lilikuwa halijadili maoni ya wananchi.
KINANA AKATIZA ZIARA ZA MWIGULU
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana anadaiwa kuwa amepiga marufuku ziara zinazofanywa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba.Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida amekuwa akifanya ziara za kuzunguka wilaya na mikoa mbalimbali kwa kutumia usafiri wa helikopta.Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini, maswahiba wake walidai kuwa wameona barua ambayo Mwigulu ameandikiwa na Kinana ya kumtaka kuacha kufanya ziara hizo mara moja.Kwa mujibu wa marafiki hao wa Mwigulu ni kwamba barua hiyo ya Kinana kwa sehemu kubwa inaeleza namna ambavyo amekuwa akifanya ziara nyingi katika mikoa na wilaya bila ushirikishwaji kamili wa makao makuu, mikoa na wilaya hasa kamati za siasa.“Nimeona ile barua ambayo Mwigulu amenitumiwa, kuna sehemu inaeleza wazi kuwa kwa kauli na matendo yake ameonesha kujiandaa kugombea nafasi ya wewe, pia umeshaonesha kwa kauli na matendo yake kujiandaa kugombea nafasi ya urais kupitia CCM.“Na kwamba ziara anazofanya mikoani na wilayani zinamuelekeo wa kampeni, jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya chama,” alisema mmoja wa rafiki wa karibu wa Mwigulu wakati akizungumzia barua hiyo.Alidai pamoja na maelezo mengine yaliyomo kwenye barua hiyo ya Kinana kwa Mwigulu kuna eneo ambalo anaagizwa kusitisha ziara zote na iwapo atataka kufanya ziara yoyote ya kichama itabidi apate kibali chake na kutakiwa kutekeleza maagizo hayo mara moja.Kwa mujibu wa marafiki hao wa Mwigulu ni kwamba sababu za kufahamu kama kuna barua ya onyo amepewa ni kutokana na kulalamikia kupewa barua hiyo. Hata hivyo, hawakuwa tayari kueleza kama amekubali kusitisha ziara zake au la.Wakati kukiwa na taarifa hizo za Kinana kumpiga ‘stop’ Mwigulu kufanya ziara hizo baadhi ya wadau wa siasa wamekuwa wakihoji wapi anakopata fedha kwa ajili ya kukodi helikopta anayotumia kwenye ziara zake kwa kuzunguka mikoa mbalimbali.Pamoja na hayo, Mwigulu ameendelea na ziara zake katika maeneo mbalimbali ambapo juzi alikuwa mkoani Tanga kabla ya kwenda Morogoro.Hata hivyo, Mwigulu hakuweza kuelezea kama amepewa barua na Kinana inayomtaka asitishe ziara zake.
KIKWETE AFUNGUA KIKAO CHA KAMATI KUU CCM ZANZIBAR
Wakati Kamati Kuu ya chama tawala,
CCM ikimaliza vikao vyake mjini hapa, Katibu Mkuu wa chama hicho,
Abdulrahman Kinana amesema mambo mengi yanayozungumzwa kuhusu baadhi ya
wanachama wanaotajwa kuwania urais hayana ukweli, wala hakuna
atakayefukuzwa uanachama.
Kinana aliyasema hayo jana mjini hapa kuhusu mambo
yaliyojitokeza kwa wagombea wa nafasi za urais kabla ya kufanyika kwa
Uchaguzi Mkuu, Oktoba.
Kamati Kuu ya CCM hadi jana jioni ilikuwa ikiendelea na kikao chake kwenye ofisi kuu ya chama, Kisiwandui, Zanzibar.
Kauli ya Kinana imekuja baada ya kuwapo kwa
minong’ono kuwa baadhi ya makada waliojitokeza kutangaza ama kuonyesha
nia kuutaka urais watachukuliwa hatua, zikiwamo kutimuliwa.
“Mambo yanayozungumzwa ni mengi kuwa baadhi ya
wagombea majina yao yatakatwa. Hayo ni majungu ya kisiasa, yamelenga
kuwachokoza viongozi na chama ili wapate cha kusema.
“Chama kina utaratibu na uamuzi unaofanyika kwa vikao maalumu, hizi ni propaganda, ni uchokozi kwa chama chetu,” alisema Kinana.
Wakati Kinana akijaribu kuwaondoa hofu vigogo
wanaowania nafasi hiyo, tayari wagombea hao wamepiga kambi mjini hapa,
baadhi yao wakiendesha kampeni za chini chini, tangu kumalizika kwa
sherehe za Mapinduzi visiwani hapa juzi.
Wagombea hao wamekuwa wakipishana kuingia visiwani
na kukutana na baadhi ya wajumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM na mkutano
mkuu kila upande ukijiimarisha kisiasa kabla ya mchakato wa kumpata
mgombea wa urais kupitia chama hicho Mei mwaka huu.
Vikumbo mitaani
Katika hoteli kadhaa mjini hapa baadhi ya makada
wamekuwa wakipigana vikumbo ikiwa ni hatua ya kuweka mikakati ya
kutengeneza mazingira, hasa ya kukubalika katika chama hicho.
Hata hivyo, tofauti na vikao vingine vya chama
hicho tawala, idadi ya wapambe wa makundi yanayotajwa kuwania urais
waliofika mjini hapa imekuwa ni ndogo.
Uchunguzi katika baadhi ya hoteli juzi na jana umezishuhudia
zikiwa na nafasi, viongozi waliofika kwa ajili ya sherehe za Mapinduzi
wakitengewa nafasi kwenye Hoteli ya Serena.
Habari kutoka ndani ya chama hicho, zinasema kuwa
makada hao walianza kuwasili mjini hapa siku moja kabla ya sherehe za
Mapinduzi na kikubwa kwa baadhi yao, kilikuwa kutafuta kuungwa mkono na
wenzao wa Zanzibar.
“Wengine waliondoka jana (juzi) baada ya sherehe.
Waliobaki bado wapo katika hoteli wakijaribu kuwasiliana na watu
wanaofikiri watawasaidia katika safari yao,” alisema mmoja wa wanachama
wa chama hicho.
Mmoja wa wapambe wa mmoja wa makada wanaowania
urais, alisikika akizungumza kwa simu katika moja ya mgahawa mjini hapa
juzi usiku baada ya kutakiwa na mmoja wa wagombea kutoka Kanda ya Ziwa
wakutane.
“Mheshimiwa (akimtaja), uko wapi?, haya nakuja sasa hivi.” alisema na kisha kwenda katika hoteli aliyofikia mgombea huyo.
Makada kadhaa wanatajwa kuwania nafasi hiyo ni
pamoja na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, (Uhusiano na Uratibu) Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba, mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mbunge wa
Nzega, Dk Hamis Kigwangala, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu.
Tibaijuka akosekana CC
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anne Tibaijuka ni mmoja kati ya wajumbe wawili
walioshindwa kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya
CCM kilichofanyika Kisiwandui.
Mjumbe mwingine ambaye hakuhudhuria ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Akizungumza jana kabla ya kuanza kikao hicho
kilichoendeshwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, Kinana
alisema wajumbe hao waliomba udhuru.
Hata hivyo, Prof Tibaijuka ni mmoja wa wana CCM waliotajwa
kupewa mgawo wa fedha wa Sh1.6 bilioni katika sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Waziri huyo alivuliwa wadhifa wake na Rais Jakaya
Kikwete mwisho wa mwezi uliopita ikiwa ni moja ya utekelezaji wa
Maazimio ya Bunge waliyoyatoa mwezi Novemba baada ya kujadili ripoti ya
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu kashfa ya Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Waziri mwingine ambaye Bunge lilipendekeza avuliwe
madaraka, Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini bado anaendelea
na wadhifa wake.
Miongoni mwa ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa
kwenye kikao hicho cha siku moja ni pamoja na Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa uliofanyika mwezi uliopita , hali ya kisiasa nchini na hatima ya
wanachama wanaodaiwa kugawiwa fedha hizo.
Utulivu
Tofauti na vikao vingine ambavyo hufanyika Dodoma,
mji wa Unguja ulionekana kuwa tulivu bila pitapita za wana CCM
waliovalia sare za chama, hata katika maeneo yaliyo karibu na ofisi
hiyo, Kisiwandui.
Mapambo yaliyokuwa yakionekana mtaani na katika
ofisi za CCM yenye rangi ya kijani na njano, yaliwekwa kama sehemu ya
shamrashamra za sherehe za Mapinduzi. Pia, wajumbe wa kikao hicho wengi
wao waliokuwa wamevalia sare za chama chao, walionekana wakiingia moja
kwa moja katika jengo hilo kuanzia saa 3.00 asubuhi baada ya kusalimiana
na wenyeji wao.
Pia, magari na misafara ya viongozi ilifanya
maeneo hayo kuwa na ukimya mwingi kama vile hakuna kitu kilichokuwa
kinachoendelea kwenye ofisi hizo.
Nje ya ukumbi kulikofanyika kikao, askari polisi
na usalama wa Taifa walijipanga kwa mstari karibu na mlango na magari
yalikuwa yakiwashusha viongozi mbalimbali.
Hadi saa 11.30 jioni jana, wajumbe walikuwa hawajatoka kwa ajili ya chakula cha mchana au kupumzika.
Hata hvyo, wajumbe wa kamati hiyo walimaliza kikao
chao baadaye usiku na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema kuwa suala kubwa lililozungumzwa ni kashfa ya Escrow, hali ya
kisiasa nchini na maadili.
“Nitazungumza zaidi kesho (leo) kwa kirefu, kwa kifupi tumezungumzia hayo kwa leo,” alisema Nape akiondoka Kisiwandui.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya kikao hicho,
kilipasha kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kimsingi
amekubali kufanya uamuzi kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo la
Escrow kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge mjini Dodoma Januari 27.
Kikao hicho cha CC ni cha kwanza kufanyika mwaka
huu ambao Tanzania itachagua rais, wabunge na madiwani katika Uchaguzi
Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba. Tayari makada kadhaa wametajwa
kuwania nafasi hiyo ambapo mwaka jana chama hicho kiliwaadhibu baadhi
yao kwa madai ya kufanya kampeni kabla ya wakati.
Katibu wa NEC
Itikadi na Uenezi CCM Taifa Ndugu Nape Nnauye akitoa salaam za pongezi
kwa wananchi wa kijiji cha Kilangala B kata ya Kilangala kwa kuipa
ushindi CCM kwenye uchaguzi serikaliza mitaa uliofanyika desemba 2014,
Katika mkutano huo Nape aliwaeleza wananchi hao CCM ndio chama pekee
kinachotoa majibu kwa matatizo ya wananchi.
MAMA SALMA KIKWETE AKISHAURIANA JAMBO
MNEC wa Wilaya ya
Lindi mjini Mama Salma Kikwete akishauriana jambo na Mkuu wa Mkoa wa
Lindi Mheshimiwa Mwantumu Mahiza wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya
CCM mkoa wa Lindi
No comments:
Post a Comment