Kikao cha CC kina majukumu matatu leo ambayo ni kufikiria na kutoa
mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), majina yasiyozidi matatu
ya walioona kuwania urais wa Zanzibar ambayo imeombwa na Rais wa sasa,
Dk Ali Mohamed Shein pekee, kufikiria na kutoa mapendekezo kwa NEC
majina yasiyozidi matano ya walioomba kuwania urais wa Muungano na
kuandaa mkutano wa NEC.
Vigezo vya maadili
Kulingana
na kanuni za Uongozi na Maadili, toleo la 2012 kifungu cha 4(ii), kuhusu
taratibu za kuomba uongozi, wanachama wanaogombea uongozi ambao uteuzi
wao hufanywa na vikao vya kitaifa, watachunguzwa kwanza uadilifu wao na
chombo cha maadili cha CCM kwa ushirikiano na vyanzo vingine.
Kanuni hizo zinasema mwanachama wa CCM anapoomba uongozi katika ngazi
yoyote, itikadi na mwenendo wake vitachunguzwa kwanza na Kamati ya
Usalama na Maadili inayohusika, ndipo maombi hayo yaliyoambatanishwa na
mapendekezo ya kamati hiyo yatakapofikishwa mbele ya kikao chenye
madaraka ya kutoa uamuzi.
Ikiwa mwanachama hakupendekezwa kwa sababu ya kukiuka Katiba ya CCM,
Kanuni za CCM na sheria ya nchi, hatakuwa na haki ya kukata rufaa kwa
mtu yeyote au kikao chochote. Lakini ikiwa mwanachama atakataliwa
kugombea kwa sababu ya madhambi yake katika chama, basi ni wajibu wa
Kamati ya Usalama na Maadili kumjulisha makosa yaliyomnyima haki ya
kugombea, naye anaweza kukata rufaa kwa mujibu wa haki zake kikatiba.
Mtu yeyote anayetuhumiwa mbele ya Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi
yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana na maadili au nidhamu ya chama
atasomewa na kutakiwa kuzijibu tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa kamati
hiyo ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa maandishi, lakini hataambiwa
nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa kama imekwishajulikana mapema
kutokana na mijadala ya vikao, vyombo vya sheria au vyombo vya habari.
Kanuni ya maadili inaendelea kusema kuwa uchambuzi wa tuhuma hizo
utafanywa kwa kutumia njia mbalimbali pamoja na mashahidi
watakaopatikana.
Uchunguzi utakapokamilika na endapo
itadhihirika kwamba tuhuma zina uzito, mtuhumiwa ataitwa mbele ya kikao
cha Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika, kama ni lazima,
ili apate kuhojiwa ana kwa ana.
Pia, kanuni inasema Kamati ya
Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika itatoa mapendekezo yake kuhusu
suala hilo kwenye kikao cha uamuzi kinachohusika. Mtuhumiwa atapewa
nakala ya uamuzi kwa maandishi.
Wagombea wanne kukosa CC
Katika kikao cha CC kinachofanyika leo, wajumbe wanne ambao ni miongoni
mwa majina 38 yatakayojadiliwa katika mchujo huo watalazimika kukaa
kando ili kukwepa mgongano wa masilahi.
Wajumbe hao ni Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro,
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal na Waziri wa Kilimo na Chakula,
Stephen Wasira.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa
CCM katika Vyombo vya Dola, Toleo la Pili – Februari, 2005, ukurasa wa
25, kifungu cha 21 (3); wajumbe wa vikao vya uchujaji na uteuzi wa
wagombea kwa ngazi inayohusika hawaruhusiwi kuendelea na kazi ya
uchujaji na uteuzi iwapo wao ni wagombea katika ngazi hiyo.
Kanuni hiyo pia imetoa miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi wa
wagombea na wajumbe wote wanatakiwa na kanuni kuzingatia maadili na
nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi.
Kanuni hizo zinasema ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa maneno au vitendo
kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji mmoja dhidi ya
mwingine, kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na
eneo analoishi au anakotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
Pia, ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya
uongozi au mwanachama yeyote aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi au
uangalizi au uratibu wa kura za maoni, uchujaji na uteuzi, kufanya
vitendo vya ukiukwaji wa kanuni.
Kuhusu misaada, kifungu cha tano
(a) kinasema ni marufuku kwa mgombea yeyote mtarajiwa au wakala wake,
kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri kuwa ni sehemu ya
kampeni za kuwania nafasi anayoitafuta kabla ya muda rasmi wa uongozi
unaohusika haujamalizika.
Kanuni imetoa adhabu kwa watakaovunja
miiko hiyo na kwa kiongozi atakayethibitika kuivunja atavuliwa uongozi
na kwa mwanachama anayeomba kugombea nafasi yoyote atakayethibitika
kuivunja hiyo hatateuliwa kugombea nafasi anayowania.
No comments:
Post a Comment