Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) leo itawasha moto upya bungeni wakati itakaposoma ripoti maalumu
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikitarajiwa kuibua
kashfa tatu nzito ikiwamo ya misamaha ya kodi.
Kashfa nyingine
zinazotarajiwa kuibuliwa ni, ufisadi katika gharama za ujenzi wa jengo la watu
mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na
uuzaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto
Kabwe alisema kuwa, tayari kamati hiyo imepokea ripoti ya ukaguzi huo ambayo
inaonyesha ufisadi wa kutisha katika maeneo hayo matatu na mengineyo.
Masuala hayo matatu pia
yaliibuka wakati wa vikao vya kamati za Bunge vilivyomalizika Dar es Salaam
wiki iliyopita, huku bodi ya korosho ikibanwa kuhusu nyumba yake aliyouziwa
Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.
Kwa mujibu wa habari hizo,
ripoti hiyo inayoonyesha jinsi ufisadi wa kutisha ulivyofanywa katika ujenzi wa
jengo la (VIP Lounge) na Serikali inadai ilitumia Sh12 bilioni kulijenga,
lakini mthamini wa majengo ya Serikali ameeleza kuwa jengo hilo lina thamani ya
Sh3 bilioni.
Katika suala la misamaha ya
kodi, PAC imepokea taarifa kutoka kwa CAG ikionyesha kuwa misamaha hiyo
iliyokuwa imefikia Sh1.5 trilioni mpaka Juni 2013, lakini baada ya mwaka moja
misamaha hiyo imeongezeka hadi Sh1.8 trilioni mpaka Juni 2014.
“Kwa mwaka moja tu, misamaha
ya kodi imeongezeka kwa zaidi ya Sh300 bilioni. Kiasi hiki ni kama escrow
fulani (Fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, Sh306 bilioni),” chanzo cha habari
kilidokeza.
Katika vikao vya kamati
hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilieleza kuwa misamaha ya kodi imepanda
kutoka Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, chanzo
kikiwa ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa. Ilisema kati ya misamaha
hiyo, Sh676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi inayotokana na Ongezeko la
Thamani (VAT) na kuwa hali hiyo itapungua iwapo nchi itaanza kutumia Sheria ya Kodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia, TRA ilifafanua kuwa
mpaka sasa wafanyabiashara na kampuni kubwa zimefungua kesi katika mahakama ya
rufaa wakipinga kulipa kodi ambayo inafikia Sh1.7 trilioni.
Mvutano mwingine
unaotarajiwa kuibuliwa katika ripoti hiyo ni uwasilishwaji wa utata wa uuzwaji
wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Awali, hati ya nyumba hiyo
ilikuwa ya Taasisi ya Kilimo Tanzania ambayo ilifutwa mwaka 1963, kabla ya mtu
mwingine kuibadilisha hati na kuiuza kwa Koka mwaka 2011.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi
hiyo, Mudhihir Mudhihir alisema Koka aliuziwa nyumba na taasisi hiyo ambayo
haikuwa mmiliki halali.
Alisema nyumba hiyo iliuzwa
kwa Sh300 milioni na katika juhudi za bodi kufuatilia taratibu za kuirudisha,
ikagundulika kuwa hati imeshabadilishwa, kusisitiza kuwa uuzwaji wa nyumba hiyo
ulifanyika kimakosa bila kufuata sheria na taratibu.
Juzi Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue alikaririwa akiwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu
makusudio ya kuuza nyumba za Serikali na mashirika ya umma, kutokana na madeni
mbalimbali ili ziweze kukombolewa kabla ya kuuzwa.
No comments:
Post a Comment