Wezesha
kama una maoni au habari tafadhali tutumie kwa kupitia email yetu.shanellally@gmail.com
Thursday, 15 January 2015
ESCROW YAPELEKEA WAWILI MAHAKAMANI
Dar es Salaam. Tume ya kupambana na kuzuia rushwa, TAKUKURU kwa mara ya kwanza imewapandisha kizimbani watuhumiwa wawili wanaohusishwa na kashfa ya wizi wa zaidi ya shilingi Bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Watuhumiwa hao walifikishwa kwenye mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, ambapo kila mmoja anakabiliwa na shitaka moja la kula rushwa. Mshitakiwa wa kwanza kupandishwa kizimbani alikuwa ni Bwana Theophilo John Bwakea, ambaye inadaiwa kuwa February 12 mwaka 2014, alitenda kosa hilo, baada ya kupokea kiasi cha shilingi Milioni 161.7, kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya VIP Engineering an Marketing na aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya uzalishaji umeme ya IPTL, James Buchard Rugemalira. Kiasi hicho cha fedha kinachodaiwa kuwa ni sehemu ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, kilitolewa kupitia akaunti ya mshtakiwa yenye namba 00410102643901, ya benki ya Mkombozi. Mshtakiwa huyo anadaiwa kupokea fedha hizo kutoka kwa Bwana Rugemarila, ikiwa ni sehemu ya shukrani zake kwa baadhi ya wajumbe waliohusika kuandaa sera ya sekta binafsi iliwatengenezea mazingira mazuri sekta hiyo kuzalisha na kuliuzia umeme shirika la Umeme nchini, TANESCO. Mshitakiwa wa pili kupandishwa kizimbani, alikuwa ni Bwana Rugonzibwa Theophil Mujunangoma, ambaye anadaiwa mnamo February 5, mwaka 2014, kwenye jengo la Benki ya Mkombozi, Ilala alipokea rushwa ya shilingi Milioni 323.4 kutoka kwa Bwana Rugemarila. Rugonzibwa ambaye ni Mkurugenzi wa idara ya masuala ya kisheria wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi alipokea kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake yenye namba 00120102602001, kiasi kinachodaiwa kuwa ni sehemu ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow. Fedha hizo pia zinadaiwa kuwa ni shukrani kwa Rugemarila kwa Mkurugenzi huyo, kutokana na mchango wake wa kuiwezesha IPTL Tanzania Ltd, kuwa mfilisi wa muda. Hata hivyo watuhumiwa wote wamekana mashtaka hayo, yaliyosomwa mbele yao na afisa wa TAKUKURU Benard Swai. Hakimu mkazi wa Kisutu, Frank Moshi, amekubali kutoa dhamana ya shilingi Milioni 50 kwa mtuhumiwa Bakewa, ambaye ni mhandisi mwandamizi wa mamlaka ya usambazaji umeme Vijijini, REA, baada ya kutimiza masharti na kesi itasomwa tena January 29, mwaka huu. Lakini pia, Hakimu Mfawidhi Emilius Mchauru, kwa upande wake ameruhusu dhamana ya shilingi Milioni 20 kwa mtuhumiwa Rugonzibwa, ambaye hata hivyo anatakiwa kufika mahakamani Ijumaa hii, na wadhamini wake ili kukamilisha mashart ya dhamana. Tayari mwanasheria mkuu wa serikali imejiuzulu kupitia kashfa hii, huku Rais jakaya Kikwete akitengua uteuzi wa waziri wa nyumba na maendeleo ya makazi, prof Anna Tibaijuka, huku katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini Eliakim Maswi, akisimamishwa kupisha uchunguzi dhidi yake, kutokana na kuhusishwa na kashfa hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment