Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo
shahidi Jafert Kibona, ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai Morogoro, alisema Agosti 9, 2013, polisi walipata
taarifa kuwa, Sheikh Ponda angekwenda Morogoro kwenye kongamano, hivyo
waliwataka waandaaji kumsalimisha polisi kiongozi huyo.
Kibona ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai Mtwara, alisema polisi walimtaka Sheikh Ponda
kujisalimisha kutokana na kutafutwa kwa tuhuma za kutoa maneno ya kashfa
na uchochezi, Dar es Salaam na Zanzibar.
Hata hivyo, Sheikh Ponda alikaidi amri hiyo,
badala yake aliendelea kutoa maneno ya kashfa na uchochezi katika
kongamano la Morogoro, alidai shahidi huyo mahakamani hapo.
Alidai walishindwa kumkamata Ponda baada ya
wafuasi wake kumwingiza kwenye gari dogo na kumtorosha, kabla ya kupata
taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa kiongozi huyo alijeruhiwa kwa
risasi bega la mkono wa kulia.
Kibona alisema walikwenda Hospitali Mkoa wa
Morogoro, lakini hawakumkuta Ponda na siku iliyofuata walipata taarifa
kuwa amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wakili wa utetezi, Juma
Nassoro alimuuliza shahidi huyo kuhusu mtu aliyempiga risasi Ponda,
ikiwa polisi ndiyo pekee waliokuwa na silaha siku hiyo.
Aliuliza pia kwa nini polisi walishindwa kumkamata Ponda wakati hakuwa na silaha. Kesi itatajwa tena Februari 2 na 19 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment