Wezesha

kama una maoni au habari tafadhali tutumie kwa kupitia email yetu.shanellally@gmail.com

Monday, 12 January 2015

SHEIN AKEMEA MAOVU SIKU KUU YA MAPINDUZI

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna kundi au mtu mwenye uwezo wa kuipindua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) au ile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na atakayethubutu kuwaza au kupanga jambo hilo atakiona cha moto. Dk Shein alitoa msimamo huo jana wakati akifunga matembezi ya UVCCM ya kumbukumbu ya Miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, mwaka 1964 katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Maisara, mjini Unguja. Alisema si SMZ wala SMT itakayopinduliwa na kundi au mtu yeyote na kuwataka wenye mawazo hayo kusahau na kuyafuta kwani nchi zote mbili zinaoongozwa chini ya vyombo vya ulinzi na usalama na wakati wote viko makini. “Lugha za kisiasa kwenye majukwaa vipimwe kabla ya kutamkwa, wanaosema wanataka nchi yao waoneshe nchi yao iko wapi, walimpa nani, njia pekee ya kuingia madarakani ni kupitia chaguzi kuu za kidemokrasia, nje ya hapo hakuna mwenye jeuri ya kufanya lolote na jambo lisilowezekana kuvunja misingi ya Mapinduzi,” alisema Dk Shein. Dk Shein, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema Zanzibar ni nchi ya wananchi wote hivyo viongozi wa kisiasa wanaotoa matamshi ya vitisho, kejeli na ujuvi waache kufanya hivyo kwa sababu kila mmoja ana uwezo wa kusema akafahamika. Alisema Zanzibar inaongozwa chini ya misingi ya kikatiba na kisheria hakuna mtu anayeweza kumtisha mwenzake na kuwashangaa baadhi ya wanasiasa ambao wanapokuwa serikalini husema vingine na wanapopanda kwenye majukwaa ya kisiasa hubadilika na kutoa matamshi yaliyokosa nidhamu. “Matamshi ya kisiasa majukwaani yasituvuruge, sote tunaweza kusema kuliko nyie, hatuna udata wa kutuzuia maneno yasitoke vinywani kwa ufasaha, acheni vitisho na kebehi ambazo hazitasaidia kujenga nchi na kuwaletea maendeleo kwa waliotupa dhamana ya kuongoza,” alieleza Dk Shein. Alisema tofauti za kisiasa na kiitikadi zisiivuruge nchi au kuvunja misingi ya amani na utulivu uliopo huku akisema hatapambana na mtu kwa maneno, aghalabu hupenda kutatua jambo gumu kwa njia ya mijadala na majadiliano mezani bila vitisho. Rais huyo wa Zanzibar alisema Mapinduzi ya Zanzibar ndiyo yaliyowapa fursa wananchi wanyonge wa Zanzibar waliotawaliwa kwa miaka mingi na wageni, hivyo ni jukumu la kila mmoja kutambua Mapinduzi ndiyo chimbuko la Uhuru kamili. Hata hivyo, aliwataka UVCCM kutekeleza mikakati yao ya kurudisha majimbo yaliyo chini ya upinzani huko Pemba na kuwataka waongozwe na nguvu ya hoja, kuelezea mafanikio yaliyoletwa na SMZ sanjari na kuwaelimisha wananchi kuendelea kuzitegemea sera za Chama Cha Mapinduzi. “Nendeni mahali popote mkafanye siasa, kazi za siasa hazina msimu, fuateni utaratibu na heshimuni sheria, mtakapokwama tuambieni tutawasaidia, kufanya siasa Unguja, Pemba na mahali popote ni ruksa kwa mujibu wa sheria, chapeni kazi msitishwe na mtu yeyote,” alisisitiza Dk Shein. Alisema kwa asili watu wa visiwa mahali popote duniani ni wahamiaji kutoka maeneo mengine Bara na hivyo Zanzibar ina mnasaba wa kidugu na damu na wenzao wa Bara na hiyo ndiyo historia ya kila kisiwa kuwa na mchanganyiko wa watu, rangi, tamaduni na makabila. “Sote tuheshimu sheria zilizopo, kauli za vitisho au kejeli dhidi ya Mapinduzi zikizidi wenye Mapinduzi yao hawatavumilia, eleweni tunaweza kubadili mfumo wa uendeshaji wa serikali na si tegemeo la CCM ishindwe uchaguzi wowote na wengine waje kushika madaraka,” alisema Rais huyo. Akizungumza kabla ya kumkaribisha Dk Shein, Mwenyekiti wa UVCCM Sadifa Juma Khamis alisema Zanzibar kuna matatizo yanayotokana na mabaki ya utawala wa Mfalme na familia yake tofauti na wakoloni wengine waliohama Afrika na kutawala katika nchi nyingine. Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alisisitiza haja na umuhimu wa Zanzibar kuandika upya katiba yake na kueleza kuwa wananchi wa Zanzibar hawajapata fursa ya kuandika Katiba iliyotokana na ridhaa yao tangu yafanyike Mapinduzi.



CHINI NI PICHA ZA MUHESHIMIWA RAIS JAKAYA KIKWETE AKISALIMIANA NA VIONGOZ WASASA NA WASTAAFU KATIKA SHEREHE ZA MAPINDUZI






No comments:

Post a Comment