JESHI
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu 510
wakiwemo viongozi watatu wa kundi linalojihusisha na uhalifu la ‘Panya
Road’ .
Watu hao wamekamatwa katika operesheni inayoendeshwa na jeshi hilo, kupambana na uhalifu.
Kamanda
wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema jana kuwa watuhumiwa
hao, ni pamoja na watuhumiwa 36 waliokamatwa juzi, kufuatia vurugu
iliyotokea Ijumaa iliyopita.
Alisema
chimbuko la Operesheni hiyo, inayoendeshwa na wakuu wa Polisi wa Mikoa
ya Kipolisi ya Temeke, Kinondoni na Ilala, wapelelezi na askari wa
kiintelijensia ni matukio yaliyowahusisha vijana hao na kusababisha
tafrani kwa wananchi mbalimbali wa jiji la Dar es Salaam.
Alitaja
viongozi wa kundi hilo wanaoshikiliwa kuwa ni Khalfani Said (24) na
Said Mohammed (22), wakazi wa Tandale Sokoni katika Manispaa ya
Kinondoni na Mohammed Nangula (19), mkazi wa Mburahati kwa Jongo, pia
Kinondoni.
Alisema kwamba kazi yao kubwa ni kuwaunganisha na kuratibu uporaji katika maeneo mbalimbali.
Alisema
mbali na ‘Panya Road’, operesheni hiyo ambayo itakuwa ya kudumu kuanzia
sasa, imewakamata wapigadebe, wacheza kamari na watuhumiwa wengine
waliokamatwa katika vijiwe na katika msako wa nyumba kwa nyumba.
“Imegundulika
kwamba kila inapotokea kijana ameuawa, wakati wa maziko viongozi hawa
wanakuwepo na kuwachochea vijana wenzao kufanya vurugu, kama ilivyotokea
Januari 2 katika eneo la Magomeni Kagera ambapo vijana walipambana na
polisi baada ya maziko ya kijana mwenzao aliyefariki kutokana na matukio
ya wananchi kujichukulia sheria mkononi Januari Mosi eneo la
Mwananyamala.
“Tunashukuru
kwa kuwa baadhi ya wananchi waliweza kutupa ushirikiano wa moja kwa
moja kuwabaini wahalifu tunaowashikilia, ni ukweli usiopingika kuwa
vijana hawa wanaojihusisha na vitendo viovu wanafahamika kwa wananchi
hivyo ni jukumu la wazazi, walezi katika mitaa yote ya Dar es Salaam
kujihusisha kikamilifu katika kuwabaini vijana hao ili tuweze kukomesha
maovu yao ambayo pia ni kero kwa wananchi,” alisema Kamanda Kova.
Aidha,
alisema katika operesheni hiyo, pia watuhumiwa hao walikamatwa na
vilevi mbalimbali zikiwemo bangi, lita 150 ya pombe kali aina ya gongo
na mabunda matatu ya dawa za kulevya aina ya mirungi.
Alisema
katika kuhakikisha msako huo unazaa matunda, jeshi hilo limeweka mpango
maalumu wa kuwahusisha moja kwa moja watendaji kuanzia ngazi ya Mitaa,
Kata na Tarafa ili waweze kushirikiana na polisi kuweza kuwabaini
wahalifu au makundi ya uhalifu wa aina hiyo.
Alisema
mpango huo utafanikiwa kutokana na semina elekezi iliyotoa mafunzo
hayo, iliyofanyika hivi karibuni kwa watendaji hao katika kukabiliana na
matukio hayo.
Aliwataka
vijana ambao hawana kazi za kufanya, kutafuta njia nyingine za
kuendesha maisha yao na siyo kujiingiza katika matumizi ya dawa za
kulevya na kufanya makosa ya jinai, yanayowafanya baadhi kujiingiza
katika makundi hayo.
No comments:
Post a Comment