Wezesha

kama una maoni au habari tafadhali tutumie kwa kupitia email yetu.shanellally@gmail.com

Sunday, 12 July 2015

URAIS 2015 MAGUFULI KUPEPERUSHA BENDERA YA CCM

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimemchagua kwa kura nyingi Dk. John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais kupitia chama hicho baada ya kufanyika mchujo mkali dhidi ya wagombea wengine 38. Magufuli aliyepita michujo yote hadi kufikia hatua ya tatu bora, amechaguliwa kwa kura 2104 sawa na asilimia 87% akifuatiwa na Balozi Amina Ali aliyepata kura 253 sawa na asilimia 10.5% na Dk. Asha Migiro aliyepata kura 59 sawa na asilimia 2.4 % ya kura zote.  Akitangaza matokeo hayo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na msimamizi wa kura, Anne Makinda, amesema kura zilizopigwa ni 2422 huku kura 6 zikiwa zimeharibika na kura zilizobaki zilikuwa 2416. Amesema mgombea huyo ndiye aliyechaguliwa na mkutano huo kwa ajili ya kupeperusha bendera ya chama hicho. Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Mjini Dodoma usiku wa kuamkia leo Julai 12, 2015, umemchagua Dk. Magufuli dhidi ya wanachama wengine ambao walipita katika mchujo wa tano bora. Matokeo ya watu watano yalimpa Dk. Magufuli kura 290, Balozi Amina Ali 284, Asharose Migiro 280, January Makamba 124 na Bernard Membe aliyejipatia kura 120. Matokeo hayo yameanza kuwekwa wazi kupitia mtandao wa kijamii wa JamiiForums, kwamba Dk. Magufuli amechaguliwa na wajumbe wa Mkutano Muu kwa zaidi ya watu 2,000 ili aweze kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao unaotegemewa kufanyika Oktoba 25, 2015. Tangu kuanza kwa mchakato wa kumpata mtu atakayepeperusha bendera ya chama hicho, mambo mengi yameibuka baada tu ya makada wake walioingia kwenye tano bora kupitia Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho akiwemo Bernard Membe, Dk. John Magufuli, Balozi Amina Ali, Asha Migiro na January Makamba wajumbe hao wa CCM walionekana kujigawa kwa namna mbalimbali, hali inayotajwa kumrahisishia Dk. Magufuli kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho kiurahisi. Kambi za wagombea wengine ndani ya chama hicho wameonekana kushikwa na butwaa tangu majina ya wagombea wao kushindwa kuingia hata tano bora, huku baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wakieleza kuwa CCM wamechukua maamuzi magumu ya kubadili upepo tofauti na watu walivyodhani. Awali ndani ya ukumbi wa mkutano, kulidaiwa kuwepo kwa mpango wa wafuasi wa kambi mbalimbali za kutaka kumpitisha Balozi Amina Ali, ili chama hicho kipate changamoto nyingi katika kumnadi mgombea huyo dhidi ya wagombea wengine wa vyama pinzani. Dk. Magufuli ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki na Waziri wa Ujenzi, alizaliwa Oktoba 29, 1959 Wilayani Chato – wakati huo ikiwa Mkoa wa Kagera (sasa Mkoa wa Geita). Dk. Magufuli ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwaka 1991 – 1994, alisoma Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza. Mwaka 1985 – 1988, alisoma Shahada ya Kwanzaya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemia na Hisabati. Hata hivyo, Mwaka 1981 – 1982, alisomea Diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati. Mnamo mwaka 1979 – 1981, alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa, Iringa. Mwaka 1977 – 1978, alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza. Mwaka 1975 – 1977, alisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera, Mwaka 1967 – 1974, alisoma Shule ya Msingi, Chato. Kwa upande wa mafunzo, Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma, Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha, Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma. Mathalani, uzoefu wa kazi wa Dk. Magufuli, mwaka 2010 – hadi sasa Waziri wa Ujenzi ambapo mwaka 2008 – 2010, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki, na mbunge wa jimbo hilo hilo, mwaka 2005 – 2008, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwaka 2000 – 2005, Waziri wa Ujenzi, mwaka 1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi, mwaka 1989 – 1995, Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) – Mwanza, mwaka 1982 – 1983, Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati).

No comments:

Post a Comment