Wezesha

kama una maoni au habari tafadhali tutumie kwa kupitia email yetu.shanellally@gmail.com

Thursday, 22 January 2015

SIWATAMBUI CHENGE NA NGEREJA ASEMA MAKINDA

Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hawatambui wenyeviti wa kamati tatu za kudumu za Bunge ambao Bunge liliazimia wavuliwe nyadhifa zao kutokana na kutajwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Pamoja na kuwapo kwa maagizo ya Bunge, baadhi yao wanaendelea kujinasibu kuwa bado ni wenyeviti huku mmoja wao akiongoza vikao vya kamati.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makinda alisema anachofahamu ni kuwa wenyeviti hao tayari wamaeshajiuzulu na kamati zao zinatakiwa kufanya uchaguzi wa wenyeviti wengine.
Wanaotakiwa kuachia nyadhifa zao ni Victor Mwabalaswa (Nishati na Madini), Andrew Chenge (Bajeti) na William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), ambaye hadi jana mchana alikuwa akiongoza kikao cha kamati hiyo.
Siku tano zilizopita Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alieleza kuwa kamati hizo zinatakiwa kufanya uchaguzi na kwamba wenyeviti hao hawakutakiwa kuongoza vikao, lakini hadi jana, hakuna uchaguzi wowote uliokuwa umefanyika na baadhi wanaendelea na majukumu yao.
Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge katika azimio lake la tatu, liliazimia kuwa watu walioshiriki katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow wakiwamo viongozi wa kamati hizo tatu, wachukuliwe hatua kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 27.
Ngeleja alikaririwa na gazeti hili hivi karibuni akisema kwamba anaendelea kushikilia nafasi hiyo kwa maelezo kuwa uchunguzi sakata hilo bado unaendelea na ikithibitika ndipo Bunge litachukua uamuzi ambao alisema atakuwa tayari kuutekeleza.
Bunge lapata msaada
Katika hatua nyingine, Makinda amesema Bunge litaanza kutumia vifaa teknolojia kuwasilisha taarifa mbalimbali na kuachana na utaratibu wa kudurufu nyaraka nyingi ili kuepusha gharama.
“Bunge linatumia zaidi ya Sh1 bilioni kudurufu miswada na nyaraka nyingine za wabunge. Sasa tunataka kutumia mfumo wa kisasa. Kila kitu kitakuwa katika kompyuta za wabunge,” alisema.
Kauli ya Makinda imekuja wakati akishukuru baada ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali vya mawasiliano na kazi kutoka Serikali ya China.
Balozi wa China nchini, Lu Youqing alimpatia Spika Makinda misaada ya vifaa hivyo vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) vyenye thamani ya Dola100,000.

No comments:

Post a Comment