Wezesha
kama una maoni au habari tafadhali tutumie kwa kupitia email yetu.shanellally@gmail.com
Monday, 9 February 2015
PINDA AITAKA KADHI
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa sababu za Bunge kutojadili suala la Mahakama ya Kadhi kuwa ni kutokana na kutoa muda zaidi kwa kamati husika ziweze kupitia na kutoa ushauri.Hata hivyo, alisema kuwa Muswaada huo pamoja na miswaada mingine itapata nafasi ya kujadiliwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge uliopangwa kufanyika kuanzia Machi 17.Pinda, ambaye aliahidi wakati wa Bunge Maalum la Katiba kuwa Muswada wa Sheria ya Mahakama ya Kadhi ungewasilishwa kwenye Bunge lililomalizika jana, alitoa kauli hiyo kwenye hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge la 10 la Muungano ambalo sasa limebakiza mikutano miwili kwa mujibu wa sheria kabla ya kukamilisha kipindi cha uhai wake.Mbali na Muswada wa Mahakama ya Kadhi, Waziri Mkuu aliitaja miswada mingine kuwa ni wa Sheria ya Kodi ya Mwaka 2014 na Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013.Akizima mjadala kuhusu Mahakama ya Kadhi kutokuwapo kwenye Rasimu ya Katiba wakati wa Bunge la Katiba mwaka jana, Pinda aliahidi kusimamia suala la kuwasilishwa muswada huo uli uwasilishwe bungeni.Hata hivyo, kumekuwa na mvutano na hali ya sintofahamu kwani baadhi ya watu walionekana kutokukubaliana na muswaada huo tangu ukiwa kwenye ngazi ya vikao vya kamati za Bunge, kutokana na gharama za kuendesha taasisi hiyo.Kuhusu fedha zilizorejeshwa kwenye ununuzi wa rada, Pinda alisema fedha hizo, Sh12.3 bilioni zitapunguza uhaba wa madawati kwa asilimia 5.1 katika shule za msingi na sekondari nchini.Fedha hizo zilirudishwa nchini zikiwa ni kiwango ambacho kampuni ya BAE System ya Uingereza ilizidisha kwenye bei ya rada baada ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza kubaini kuwapo na ufisadi katika mchakato mzima wa kununua kifaa hicho.Pinda alisema fedha hizo ambazo zilitolewa kwenye halmashauri mbalimbali nchini mpaka sasa zimeshatumika kusambaza madawati ya plastiki 30,996 nchini nzima.Alisema usambazaji wa madawati 61,468 ya mbao utaanza hivi karibuni na kwamba Serikali imekamilisha mikataba ya kusambaza madawati mengine 75,699 ya plastiki.“Katika mwaka 2014/2015, kiasi cha Sh1.1 bilioni kimetengwa na halmashauri kwa ajili ya kununua madawati 152,000,” alisema Pinda.Mtendaji huyo mkuu wa Serikali alisema shule za msingi nchini zina upungufu wa madawati milioni 1.2, huku za sekondari zikihitaji madawati 120,000.Katika hatua nyingine, kiongozi huyo aliwaagiza wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri ambazo bado ziko katika ujenzi wa maabara, wafanye haraka kwa kuwa Rais hayuko tayari kuongeza muda zaidi wa ule wa Juni aliouweka.Alitaja baadhi ya mikoa ambayo iko nyumba katika ujenzi wa maabara kuwa Rukwa, Kigoma, Dodoma, Tabora na Lindi huku mikoa ya Njombe, Ruvuma na Morogoro ndiyo iliyofanya vizuri zaidi katika ujenzi huo.Waziri Mkuu alieleza kuwa bado kuna changamoto kubwa ya upungufu madawati kwa shule za msingi na sekondari na kwamba zinahitajika juhudi za makusudi kwa ajili ya kumaliza tatizo hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment